|
|
NEWS(HABARI)
VIONGOZI WA AFRIKA MASHARIKI WATOA WITO WA KUSITISHWA KWA MAPIGANO MASHARIKI MWA DR CONGO
Wakuu wa nchi za Afrika Mashariki wametoa wito wa kusitishwa mara moja mapigano na kusitishwa kwa uhasama kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na makundi kadhaa ya waasi wanaopigana katika eneo lake la mashariki.
Katika mkutano uliofanyika katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi, viongozi hao pia waliagiza kwamba makundi ya waasi yaachie maeneo yote wanayoshikilia, na kwamba mazungumzo ya amani yaimarishwe.
Wakuu wa jeshi la kanda pia waliwaeleza marais juu ya taratibu za uendeshaji na sheria za ushiriki wa kikosi cha kijeshi cha Afrika Mashariki, ambacho kitatumwa hivi karibuni katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Ituri ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Mkutano huo pia umelaani matukio ya hivi karibuni ya matamshi ya chuki na mashambulizi dhidi ya makabila fulani nchini DR Congo, yanayodaiwa kuchochewa na shutuma kutoka DR Congo kwamba Rwanda inawaunga mkono waasi wa M23.
Kikosi hiki kitakachofanya kazi sanjari na jeshi na vikosi vya utawala vya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kitakuwa chini ya uongozi wa Kenya.
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Kenya, Jenerali Kibochi ndiye mwenyekiti wa Kamati ya wakuu wa kijeshi wa nchi hizi.
Kulingana na taarifa ya pamoja iliyotolewa na ofisi ya rais wa Kenya, kikosi hicho kitaundwa kwa mujibu wa itifaki kuhusu amani na usalama pamoja na Kifungu cha 125 kuhusu ushirikiano katika ulinzi.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo tayari imeidhinisha kujiunga kwa Mkataba huo- kwa itifaki zote ikiwa ni pamoja na ile ya amani na usalama.
Kundi la M23, mojawapo ya vikundi vingi vilivyoko Kivu Kaskazini, liliibuka kwa mara ya kwanza mwaka 2012 na kudai kuwa linapigania haki za Watutsi wa kabila la Kongo. Mapigano kati yao na vikosi vya serikali yameongezeka tangu Machi, na wiki iliyopita, waliteka mji wa Bunagana kwenye mpaka na Uganda.
|